Revelation of John 18

Kuanguka Kwa Babeli

1 aBaada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mng’ao wake. 2 bNaye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema: “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu!
Umekuwa makao ya mashetani
na makazi ya kila pepo mchafu,
makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.

3 cKwa maana mataifa yote yamekunywa
mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.
Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao,
nao wafanyabiashara wa dunia
wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”

4 dKisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,
ili msije mkashiriki dhambi zake,
ili msije mkapatwa na pigo lake lolote;

5 ekwa kuwa dhambi zake zimelundikana hadi mbinguni,
naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.

6 fMtendee kama yeye alivyotenda;
umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda.
Katika kikombe chake mchanganyie
mara mbili ya kile alichochanganya.

7 gMpatie mateso na huzuni nyingi sawa na
utukufu na anasa alizojipatia.
Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,
‘Mimi ninatawala kama malkia;
mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’

8 hKwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:
mauti, maombolezo na njaa.
Naye atateketezwa kwa moto,
kwa maana Bwana Mwenyezi Mungu amhukumuye ana nguvu.

9 i“Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea. 10 jKwa hofu kubwa ya mateso yake, watasimama mbali na kulia na wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
ee Babeli mji wenye nguvu!
Hukumu yako imekuja katika saa moja!’

11 k“Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena: 12 lBidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marmar, 13 mbidhaa za mdalasini, vikolezi, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ng’ombe na kondoo; farasi na magari; na miili na roho za wanadamu.

14“Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’ 15 nWale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema:
16 o“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi,
ya rangi ya zambarau na nyekundu,
ukimetameta kwa dhahabu,
vito vya thamani na lulu!

17 pKatika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa
kama huu umeangamia!’

“Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali.
18 qWatakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ 19 rNao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
mji ambao wote wenye meli baharini
walitajirika kupitia kwa mali zake!
Katika saa moja tu ameangamizwa!

20 sFurahia kwa ajili yake, ee mbingu!
Furahini watakatifu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu
kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ”

21 tKisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema: “Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli
utakavyotupwa chini kwa nguvu
wala hautaonekana tena.

22 uNyimbo za wapiga vinubi na waimbaji,
wapiga filimbi na wapiga tarumbeta
kamwe hazitasikika tena ndani yako.
Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi
mwenye ujuzi wa aina yoyote.
Wala sauti ya jiwe la kusagia
kamwe haitasikika tena.

23 vMwanga wa taa
hautaangaza ndani yako tena.
Sauti ya bwana arusi na bibi arusi
kamwe haitasikika ndani yako tena.
Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.
Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.

24 wNdani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu
na wote waliouawa duniani.”
Copyright information for SwhKC